Usajili

Uandikishaji wa waajiri na wanachama ni jambo muhimu sana kwani linasaidia LAPF kuwa na takwimu na kumbukumbu sahihi za wanachama ikiwa ni pamoja na umri, jinsia, tarehe ya kustaafu, kiwango cha michango, wategemezi n.k. Katika mfumo wa pensheni ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi kwani zinasaidia katika kufanya tathmini ya Mfuko na kujua uwezo wake katika kutoa au kuboresha mafao.

Uandikishaji wa Waajiri

LAPF huwaandikisha Waajiri kwa kuwasajili kupitia fomu Na. LAPF/REG.l. Baada ya kujiandikisha mwajiri hupatiwa hati ya usajili ijulikanayo kama LAPF/REG.2 ambayo huwajibika kuiweka mahali panapoonekana katika ofisi yake. Baada ya usajili, mwajiri mchangiaji anawajibika kufanya mambo yafuatayo:

  • Kutoa kumbukumbu sahihi za watumishi ambazo zitatumika katika uandikishaji na ulipaji wa mafao;
  • Kuhakikisha kwamba watumishi wote walioandikishwa na LAPF wanachangia na michango yao inawasilishwa kila mwezi pamoja na       vielelezo vya michango hiyo (Deduction details);
  • Kuhakikisha watumishi wote waliojiandikisha na LAPF wanajaziwa data-sheet na kuwekewa deduction code No. 639 kwenye mfumo wa kompyuta wa LAWSON (kwa watumishi wa umma wanaolipwa mishahara kupitia Hazina);
  • Kupitia mara kwa mara payroll kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanachama wote wa LAPF wanachangia;
  •  Kuiarifu LAPF juu ya mabadiliko yeyote yanayomhusu mtumishi kwa mfano kubadilika kwa majina na taarifa nyingine muhimu za mtumishi;
  • Kuwasilisha orodha ya wanachama wanaolipwa mishahara kutoka vyanzo vya ndani vya Mwajiri iIi kuweza kutambuliwa na LAPF.
Uandikishaji wa Wanachama
Jukumu la kuwaandikisha wanachama kwenye Mfuko linaihusu LAPF, mwajiri pamoja na wanachama wenyewe. Kwa mujibu wa Sheria ya LAPF, kifungu Na. 16 na 17 majukumu ya kila mmoja yameelezwa wazi. Aidha, Sheria Na.8 ya mwaka 2008 ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii, kifungu cha 30 imetamka kuwa "Mfanyakazi ambaye hajawahi kujiunga na Mfuko wowote wa pensheni au anayeajiriwa kwa mara ya kwanza anao uhuru wa kuchagua na kujiunga na Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii aupendao". Kwa msingi huo LAPF kama ilivyo mifuko mingine ina jukumu la kuwaelimisha watumishi wapya iIi waweze kuamua mfuko wa kujiunga baada ya kuelewa huduma na mafao yanayotolewa. Wanachama wa LAPF wako katika makundi mawili ambayo ni wanachama wa lazima na wanachama wa hiari.

 

Wanachama wa Lazima

Mwanachama wa lazima ni yule ambaye yuko katika ajira ya kudumu au ya mkataba akipokea mshahara kila mwezi. Mwanachama katika kundi hili anawajibika kuchangia katika mfumo wa lazima hivyo atajaza fomu ya uandikishwaji wa LAPF ijulikanayo kama LAPFIREG.3A na kupatiwa nambari ya uanachama na kitambulisho (LAPFIREG.4) ambacho kitatumika kujitambulisha wakati wa mawasiliano na LAPF na baadae katika ulipaji wa mafao.

Wanachama wa Hiari

LAPF inao pia mpango wa akiba wa hiari ambao mwanachama wake ni mtu yeyote aliyeamua kujiwekea akiba. Kundi linalohusika katika mpango huu ni wale ambao wamejiajiri wenyewe (wakulima, wavuvi, waendesha pikipiki, wasanii, wafanya biashara ndogondogo n.k.) Watumishi wanaochangia katika mfumo wa lazima wanaweza pia kuchangia kwa ziada katika mpango huu. Chini ya mpango huu uanachama utakamilika baada ya mwanachama kujaza fomu ya LAPF (LAPF/REG.3B) na kupatiwa nambari ya uanachama na kitambulisho (LAPF/REG.4). Mwanachama ataelekeza kiasi ambacho yuko tayari kuchangia kwa mwezi, kwa wiki na hata kwa siku, iIi mradi jumla yake isiwe chini ya shilingi 20,000/= kwa mwezi