Historia ya LAPF

Mfuko wa Pensheni wa LAPF ulianzishwa mwaka 1944 na iliyokuwa Serikali ya Kikoloni ya Tanganyika kwa ajili ya Wafanyakazi wa ngazi za chini kama vile Maakida na Makarani kwa lengo la kuwawezesha kujiwekea akiba.

Baada ya uhuru LAPF iliendelea kutoa huduma ya hifadhi ya jamii kwa watumishi wa Serikali za Mitaa. Mwaka 1972 Serikali ilisitisha shughuli za Serikali za Mitaa na kuzihamishia Mikoani chini ya mpango wa Madaraka Mikoani. Kufuatia hatua hii shuguli za LAPF zilisimama hadi Serikali za Mitaa ziliporejeshwa chini ya kifungu Na.16 cha Sheria Na. 10 ya mwaka 1982. Kwa kipindi chote LAPF ilikuwa ikifanya kazi kama kitengo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mnamo mwezi Julai mwaka 2000 LAPF ilifanywa kuwa taasisi inayojitegemea chini ya Bodi ya Wadhamini kupitia Sheria Na.6 ya mwaka 2000. Kutokana na tofauti za mafao kati ya watumishi wa Serikali za mitaa na wale wa Serikali kuu Serikali ilisikia kilio cha watumsihi wa Serikali za mitaa kwa kufanya mabadiliko ya mfumo wa LAPF kuwa wa pensheni. Mabadiliko hayo yalifanywa kwa Sheria Na. 9 xa mwaka 2006 na kufuatia mabadihko hayo kanuni ya ulipaji mafao inafanana na ile inayotumika kwa watumishi wa Serikali kuu.

Mwaka 2008 Serikali ilitunga Sheria ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (The Social Security Regulatory Authority Act No.8 of 2008) ambayo pamoja na mambo mengine ilitoa uhuru wa watumishi wapya kuamua mfuko wa kujiunga. Kufuatia Sheria hiyo LAPF sasa inaandikisha wanachama toka kwenye sekta zote za uchumi hapa nchini ikiwa ni Serikali kuu, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umma, makampuni binafsi, taasisi za elimu, makampuni ya kimataifa, asasi za kiraiya n.k. IIi kutoa mafao yaliyo bora LAPF imejiwekea Dira na Dhamira endelevu inayolenga kuleta tija na ufanisi katika utendaji kazi. DIRA ya LAPF ni Kuwa Mfuko Bora wa Pensheni unaopendwa zaidi hapa Tanzania.